Mama taifa Rachel Ruto, amesema uwekezaji katika sekta za kilimo na biashara ni nguzo muhimu katika kukuza ajenda ya mabadiliko ya Kenya.
Akihutubia kikao cha wanabiashara mjini Edoret, kaunti ya Uasin Gishu, mama taifa alisema sekta hizo mbili ni muhimu katika ustawishaji wa taifa.
Bi. Ruto aliwahimiza wakenya kumuunga mkono Rais katika ajenda kuu za serikali za ukuzaji uchumi zikiwemo nyumba za bei nafuu, dijitali na Ubunifu.
“Tumuunge mkono Rais wetu katika maswala aliahidi ikiwa ni pamoja na nyumba za gharama nafuu, mtandao wa kidijitali, huduma za afya kwa wote, kilimo na uchumi,” alisema Mama taifa.
Alihimiza jamii ya wanabiashara kujiwiainisha na mpango wa serikali wa kuwainua walio chini.
“Rais wetu amejitolea kuhakikisha ahadi alizotoa zinaafikiwa hasa ajenda ya mfumo wa uchumi wa bottom-up, ” aliongeza Mama taifa.
Kadhalika mama taifa alisema kwamba, rais amejitolea kuhakikisha ahadi zilizotolewa kwa wakenya zinatimizwa.
Miongoni mwa waliohudhuria mkutano huo ni pamoja na Seneta mteule Veronica Maina na Selina Bii ambaye ni mke wa Gavana wa Uasin Gishu.
Wengine ni Willy Kenei, mwenyekiti wa chama cha wanabiashara wa Eldoret, Felix Kiili, mwenyekiti wa chama cha wakulima, Spika wa bunge la kaunti ya Uasin Gishu na viongozi wa kidini miongoni mwa wengine.