Home Habari Kuu PSC: Hatujamteua Maribe kuwa Mkuu wa Mawasiliano

PSC: Hatujamteua Maribe kuwa Mkuu wa Mawasiliano

0

Tume ya Utumishi wa Umma, PSC imekanusha madai kuwa imemteua mwanahabari Jacque Maribe kuwa Mkuu wa Mawasiliano katika Wizara ya Utumishi wa Umma. 

Siku chache zilizopita, habari zilichacha katika mitandao ya kijamii kuwa Maribe ameteuliwa katika wadhifa huo na Waziri wa Utumishi wa Umma Moses Kuria.

Hata hivyo, mwenyekiti wa PSC Anthony Muchiri amebainisha kuwa uteuzi kama huo haujafanywa na tume wala bodi ya PSC haijapokea ombi la kumuajiri Maribe.

“Ili kuweka bayana, wadhifa huo utajazwa kupitia mchakato wenye ushindani ikiwa utatokea,” imesema PSC katika taarifa.

Maribe pamoja amekuwa akikabiliwa na mashtaka ya mauaji ya mfanyabiashara Monica Kimani na siku chache zilizopita, aliondolewa lawama na mahakama.

Hata hivyo, Jaji Grace Nzioka alipendekeza kuwa Maribe afunguliwe mashtaka ya kutoa taarifa za uongo, pendekezo ambalo Mkuu wa Mashtaka ya Umma Renson Ingonga ameridhia.

Ingonga ameashiria kuwa atakata rufaa dhidi ya uamuzi uliomwondolea lawama Maribe katika mauaji hayo.

Taarifa za Maribe kuajiriwa kama Mkuu wa Mawasiliano katika Wizara ya Utumishi wa Umma ziliripotiwa kutolewa na rafikiye wa dhati Dennis Itumbi kupitia akaunti yake ya mtandao wa X. Akimpongeza kufuatia uteuzi huo, Itumbi alimtakia Maribe baraka na kila la kheri katika kazi hiyo mpya.

Jana Jumatano, mshtakiwa mwenza wa Maribe na ambaye awali alikuwa mchumba wake Joseph Irungu almaarufu Jowie alihukumiwa kifo kwa kumuua mfanyabiashara Monica Kimani.

Mwanasheria wake ameashiria kuwa watakata rufaa dhidi ya hukumu hiyo.

Website | + posts