Home Burudani Profesa Jay ahojiwa kwa mara ya kwanza tangu alipougua

Profesa Jay ahojiwa kwa mara ya kwanza tangu alipougua

0

Msanii wa muziki na mwanasiasa wa Tanzania Profesa Jay amehojiwa kwa mara ya kwanza kabisa tangu alipougua mwanzo wa mwaka uliopita.

Jay ambaye jina lake halisi ni Joseph Haule alikuwa akizungumza nyumbani kwake ambapo alitembelewa na watangazaji wa kipindi cha “Power Breakfast” cha Clouds Fm ambao walifanya kipindi hicho mubashara kutoka huko.

Sauti yake ilisikika kwamba bado haijarudi sawa kama awali lakini alisema kwamba amepata nafuu sana kuliko awali alipokuwa amelazwa hospitalini.

Alishukuru Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan kwa kugharamia matibabu yake nchini Tanzania na India akisema angependa kukutana naye ili amshukuru.

Lengo la mahojiano ya leo ni kutanganza kuasisiwa kwa wakfu wake ambao utazinduliwa rasmi Novemba 24, 2023, tangazo lililotolewa wiki jana kupitia Clouds FM na mkewe Grace Mgonjo.

Jay alisema kwamba ameamua kuanzisha wakfu huo kutokana na matatizo ambayo watu wengi walio na ugonjwa wa figo wanapitia kutokana na gharama ya juu ya matibabu.

Alielezea kwamba yeye alichomwa sindano fulani iliyomsaidia sana na alichomwa mara mbili kwa siku kwa muda wa siku tano na iligharimu shilingi milioni 50.

Jay ambaye alilazwa kwenye chumba cha wagonjwa mahututi kwa siku 127, alielezea kwamba sauti yake imebadilika kutokana na hatua ya madaktari kutoboa koo ili kuvuta uchafu kutoka kwenye mapafu yake.

Website | + posts