Waziri mteule wa Usalama wa Taifa Prof. Kithure Kindiki amesema polisi walijitahidi vilivyo kudhibiti hali wakati wa maandamano ya vijana wa Gen Z.
Amesema watu 42 walifariki wakati wa maandamano hayo huku raia 486 na maafisa wa polisi 385 wakijeruhiwa.
Jumla ya watu 1,387 walikamatwa wakati wa maandamano hayo ambayo pia yalisababisha kuharibiwa kwa magari 54 ya polisi na 110 yanayomilikiwa na Wakenya.
“Kwa jumla, polisi walijaribu wawezavyo kulinda nchi dhidi ya makundi ya watu wenye fujo, wahalifu, wachomaji mali na watu wengine hatari wakiwemo wale waliovamia bunge na walitaka kuwaua wabunge,” alisema Prof. Kindiki wakati akisailiwa bungeni leo Alhamisi.
Matamshi yake yanakuja wakati mashirika ya kutetea haki za kibinadamu yamewashutumu vikali polisi kwa ukandamizaji ulioshuhudiwa dhidi ya waandamanaji wakati wa maandamano ya vijana wa Gen Z.
Mawaziri wengine wanne wateule wamepangiwa kusailiwa leo Alhamisi akiwemo Debra Mlongo Barasa (Afya), Alice Wahome (Ardhi), Julius Migos Ogamba (Elimu) na Soipan Tuya (Ulinzi).