Mwanamuziki wa Nigeria Portable hatimaye ameelezea ni kwa nini amekasirishwa na mwanamuziki mwenzake Davido.
Katika mahojiano kwenye kipindi Echo Room, Portable alisema kwamba sababu kuu ni hatua ya Davido ya kutotimiza ahadi yake hata baada ya kuacha mambo muhimu na kuwa na muda naye nchini Marekani.
Portable anasema alikuwa amekwenda kwa ziara ya kikazi nchini Marekani ambapo alikutana na Davido katika jimbo la Atlanta. Alilazimika kufutilia mbali tamasha ambalo lingempa mapato ya dola elfu 6 ili kukaa na Davido.
Anasema pia kwamba katika ziara yake nchini Marekani, alikuwa anatafuta msanii wa kimataifa wa kushirikiana naye kikazi, azma aliyokatiza baada ya Davido kuahidi kufanya naye kazi.
Sasa anasema Davido amekataa kutimiza ahadi yake na ana hasira kutokana na hasara aliyopata.
Awali, Portable alimzomea mwanamuziki mwenzake kwa jina Zlatan mitandaoni kufuatia ushauri aliompa wa kuwa makini na jinsi anahusiana na Davido.
Portable alihisi kwamba Zlatan hakuwa anamtakia mazuri ila sasa amelazimika kumwomba msamaha baada ya kutendewa mambo yasiyo ya haki na Davido.