Home Kaunti Polisi wawaruhusu wanaharakati kufanya maandamano Mombasa

Polisi wawaruhusu wanaharakati kufanya maandamano Mombasa

0

Wanaharakati wa mashirika ya kijamii mjini Mombasa wako radhi kufanya maandamano ya kuadhimisha siku ya Saba Saba keshokutwa Ijumaa. 

Hii ni baada ya kupata kibali kutoka kwa polisi.

Wanaharakati hao walikubaliwa kufanya maandamano hayo baada ya kukutana na afisa anayesimamia kituo cha polisi cha Central mjini Mombasa chini ya mwavuli wa vuguvugu la mashirika ya Kijamii ya Pwani.

Wameahidi kufanya maandamano ya amani kutoka eneo la Elephant Tusks kwenye barabara ya Moi Avenue hadi eneo la Treasury Square.

Kulingana nao, wamekubaliana na polisi kuwajibikia visa vyovyote vya vurugu vinavyoweza kutokea wakati wa maandamano hayo wakiongeza kuwa watakuwa na walinzi wao wa kibinfasi kuhakikisha amani inadumu.

Ikiwa yatafanyika, haya yatakuwa maandamano makubwa kuwahi kufanyika Pwani tangu utawala wa Kenya Kwanza kuingia madarakani.

Kinyume cha Nairobi na Kisumu, Mombasa haijakuwa ikishiriki maandamano yaliyoitishwa awali na muungano wa Azimio kuipinga serikali.

Oginga Randiki, mshauri wa mashinani wa kiongozi wa Azimio Raila Odinga huko Pwani amesema watatumia maandamano hayo kulalamikia gharama ya juu ya maisha na Sheria ya Fedha ya Mwaka 2023 anayosema iliwaongezea kodi Wakenya ambao tayari wanateseka.

“Huu ni mwanzo wa maandamano ya kuishinikiza serikali kuwapunguzia Wakenya gharama ya maisha. Hatutakoma hadi serikali hii isikilize vilio vya Wakenya wanaoteseka,” alisema Randiki.

Mkurugenzi Mkuu wa shirika la Concern Citizens Bradley Ouna alisema kuongezwa kwa ushuru thamani wa mafuta kutoka asilimia 8 hadi 16 kumeanza kuwatesa Wakenya na kuongeza gharama ya maisha.

“Tunataka kutumia maandamano kumkumbusha Rais William Ruto juu ya ahadi zake za kabla ya uchaguzi kwamba hatamwekea mzigo raia wa kawaida akichaguliwa. Sheria ya Fedha ina athari kubwa hasi kwa Mkenya wa kawaida na inapaswa kufutiliwa mbali,” alilalamika.

Muungano wa Azimio umetangazwa kufanyika kwa maandamano kote nchini Ijumaa hii kupinga kutekelezwa kwa Sheria ya Fedha ya Mwaka 2023, huku mkutano mkuu utakaohudhuriwa na vinara wa muungano ukitarajiwa kuandaliwa katika uwanja wa Kamukunji katika kaunti ya Nairobi.

Taarifa ya Eyob Mengistu Alemayehu

Website | + posts

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here