Viongozi wa eneo la Kaskazini Mashariki mwa nchi, wametoa wito kwa polisi, kuelezea aliko mwakilishi wadi wa Dela, Yussuf Hussein Ibrahim.
Wakiongozwa na mbunge wa Eldas Adan Keynan, viongozi hao walielezea wasiwasi wao kuhusu kimya kirefu tangu kutoweka kwa mwakilishi wadi huyo, wakisema familia yake inapitia wakati mgumu.
Keynan alidokeza kuwa ukosefu wa habari kutoka kwa maafisa wa polisi, ni ukiukaji wa katiba, inayotoa haki ya ulinzi kwa kila mkenya.
Viongozi hao kutoka kaunti za Wajir, Mandera, Isiolo, na Garissa, walitoa wito kwa polisi kubainisha iwapo mwakilishi wadi huyo anazuiliwa katika kituo cha polisi, au watoe habari kuhusu uchunguzi unaoendelea.
Familia ya Ibrahim, inasema kuwa alitekwa nyara katika mtaa wa South B jijini Nairobi, Septemba 13,2024.
Viongozi hao wamefika katika mahakama kuu, kumshurutisha kaimu Inspekta Jenerali wa polisi kumwasilisha mahakamani Ibrahim akiwa hai au akiwa amefariki.
Kulingana na familia ya Ibrahim, mwakilishi wadi huyo alitekwa nyara alipokuwa akisafiri kwenye taxi, katika barabara ya Enterprise Jijini Nairobi.