Maafisa wa polisi wamepata mbuzi 13 katika eneo la Wamba kaunti ya Samburu, waliokuwa wameibwa kutoka kaunti ya Laikipia.
Mifugo hao waliripotiwa kuibwa tarehe 23 mwezi Julai na kusababisha msako kuanzishwa, ukiongozwa na kaimu naibu kamishna wa kaunti ndogo ya Samburu Mashariki James Katana.
Kulingana na Katana, upatikanaji wa mbuzi hao ulifanikishwa na juhudi za pamoja za machifu na manaibu wao, wazee wenye utaalamu wa kufuata nyayo za mifugo na maafisa wa polisi wa kituo cha wamba.
“Siku ya Jumatano tarehe 26 mwezi Julai, nilipashwa habari na wakuu wa usalama upande wa laikipia na isiolo kwamba mbuzi ambao wameibwa wameingia katika eneo langu, taarafa ya Wamba. Nilichukua hatua ya haraka kuleta pamoja maafisa wa serikali, polisi na wazee wa jamii ya Samburu na tukaanza kufuata nyayo za mifugo hao. Kufika eneo liitwalo Nkiseu, washukiwa wa wizi huo wakatambua kwamba wanafuatwa ndipo wakaacha mbuzi na kutorokea msituni,” alisema kaimu naibu kamishna wa kaunti ndogo ya Samburu Mashariki James Katana.
Licha ya kuwa visa vya wizi wa mifugo vimeshuhudiwa katika kaunti za Isiolo, Samburu na Laikipia, Katana anasema kuajiriwa kwa maafisa wa polisi wa akiba, kumesababisha kupungua pakubwa kwa visa hivyo katika kaunti ndogo ya Samburu Mashariki.
“Wakati umewadia kwa wakazi wa Samburu kusitisha tamaduni potovu ya wizi wa mifugo. Nawahiza wasichana wa Samburu wakome kutunga nyimbo za kuwasifu wavulana (warani) kila mara wanapoleta mifugo wa wizi kwa manyatta. Vile vile, viongozi tushirikiane tuhamasishe jamii ya wasamburu wakumbatie elimu waache kutegemea ufugaji pekee kama njia ya kujipatia kipato,” alidokeza Katana.