Kamishna wa polisi katika jimbo la Lagos nchini Nigeria, Idowu Owohunwa amefichua kwamba kifo cha mwanamuziki aitwaye Ilerioluwa Aloba maarufu kama Mohbad kilisababishwa na pigano kali kati yake na rafiki yake wa utotoni Ibrahim Owodunni maarufu kama Primeboy.
Ung’amuzi huo unafuatia uchunguzi kuhusu kifo cha Mohbad uliokuwa ukiongozwa na kundi la wachunguzi lililoundwa na maafisa wa polisi wa Lagos.
Afisa Owohunwa katika kikao na wanahabari alisimulia kwamba Mohbad na Primeboy walipigana vibaya wakati wa tamasha moja katika eneo la Ikorodu jijini Lagos, pigano ambalo lilimsababishia Mohbad jeraha baya kwenye sikio lake.
Primeboy sasa ndiye mshukiwa mkuu wa kifo hicho cha ghafla cha Mohbad. Alijisalimisha kwa polisi baada ya kibali cha kumkamata kutolewa kwa kukosa kutii mwaliko wa awali wa polisi.
Muuguzi Feyisayo Ogedemgbe ambaye uhudumia wagonjwa nyumbani naye ni mshukiwa mkuu katika kifo hicho cha Mohbad kwa sababu anasemekana kumdunga sindano ya dawa ambayo ilimsababishia Mohbad matatizo na baadaye akaaga dunia.
Polisi wanamlaumu kwa kutoa dawa hiyo bila maelekezo ya daktari na katika mazingira ambayo sio hospitali.
Kwenye video iliyosambazwa mitandaoni ikimwonyesha Mohbad akiwa katika dakika zake za mwisho mwisho, anasikika akimtaja mwanamuziki mwenza Zinolesky akisema yeye ndiye alimsema isijulikane alimsema kwa nani na ni kuhusu nini.
Mwanamuziki mwingine kwa jina Naira Marley naye alihojiwa na polisi kuhusu kifo cha Mohbad.