Home Habari Kuu Polisi wanasa unga wa maziwa ya magendo Nairobi

Polisi wanasa unga wa maziwa ya magendo Nairobi

Kulingana na idara hiyo ya DCI, gunia moja la unga wa maziwa liliuzwa kwa shilingi 16,500.

0
Polisi wanasa unga wa maziwa ya magendo Jijini Nairobi.

Maafisa wa polisi wamenasa zaidi ya tani 32.5 za unga wa maziwa ya magendo, katika bohari iliyoko kwenye barabara ya Eastern Bypass jijini Nairobi.

Idara ya upelelezi wa jinai, DCI ilisema kuwa operesheni hiyo ilifanikiwa baada ya mtu mmoja kuelekeza mpelelezi wa idara hiyo katika eneo la Kamakis kwenye barabara hiyo. Afisa huyo alijifanya mnunuzi wakati wa operesheni hiyo.

Baada ya kuwasili, lori lililokuwa na magunia 150 ya unga huo wa maziwa liliwasili.

Kulingana na idara hiyo ya DCI, gunia moja la unga wa maziwa liliuzwa kwa shilingi 16,500, huku magunia hayo yote yakigharimu shilingi 2,475,000.

Lori hilo lilikuwa likisindikizwa na mmiliki wa maziwa hayo, aliyekuwa akiendesha gari aina ya Toyota Prado lenye nambari za usajili KDN 573V, na ambaye anaaminika huwa anawasambazia wafanyabiashara maziwa hayo Jijini Nairobi.

Maafisa hao wa DCI waliwakamata washukiwa wawili, Joseph Waweru na Ali Noor, lakini dereva wa lori hilo alifanikiwa kutoroka.

Baada ya kuhojiwa, washukiwa hao walifanikiwa kupata bohari la washukiwa hao lililoko eneo la Ruai katika barabara ya Eastern bypass.

walipoingia katika bohari hilo, maafisa hao wa polisi walipata magunia 1,150 zaidi ya unga wa maziwa, kila gunia likiwa la kilo 25, pamoja na magunia 289 ya mahindi.

Kulingana na idara ya DCI, katika bohari hilo pia kulikuwa na lori lenye nambari za usajili KDG 087Z linaloaminika huwa linasafirisha kemikali aina ya Ethanol.

Washukiwa hao wanazuiliwa na polisi huku uchunguzi zaidi ukiendelea.

Website | + posts