Maafisa wa polisi wamepata mizoga ya punda katika kichaka kimoja kaunti ya Kiambu, iliyokuwa ikitayarishwa ili kuuzwa katika masoko ya humu nchini.
Mizoga hiyo ilipatikana kufuatia msako mkali uliotekelezwa na maafisa wa polisi jana Jumatatu usiku katika kijiji cha Kiahiti, kata ndogo ya Gatune kaunti ya Kiambu.
Awali, maafisa wa polisi katika kituo kidogo cha polisi cha Nachu, walipokea habari za kijasusi kuhusu shughuli ya kuwachinja punda iliyokuwa ikiendelea na wakachukua hatua za haraka na kufika eneo hilo.
Kulingana na maafisa wa polisi, wanabiashara walaghai walilenga kuuza nyama hiyo katika maduka ya nyama jijini Nairobi kwa kisingizio kuwa ni nyama ya ng’ombe.