Majasusi wamepata mihadarati inayoshukiwa kuwa Cocaine, kwenye msako unaoendelea dhidi ya ulanguzi wa dawa za kulevya jijini Nairobi.
Kwenye oparesheni iliyotekelezwa mtaani Buru Buru mapema Alhamisi asubuhi, makachero wa kitengo cha kukabiliana na mihadarati walivamia nyumba moja katika mtaa wa Harambee na kupata tembe 18 za mihadarati hiyo inayosababisha uraibu.
Kadhalika kwenye msako huo uliotekelezwa saa kumi na mbili alfajiri, mabunda ya pesa za Kenya na zile za kigeni zinazoaminika kutokana na ulanguzi wa mihadarati yalipatikana.
Pesa hizo zilijumuisha dola 12,601 za kimarekani, euro 15, shilingi 509, 495 za Kenya, shilingi elfu- 24 za Tanzania na Kwanza elfu-10 za Angola.
Majasusi hao walisema kuwa washukiwa wawili ambao ni Curtis Muli na Teresa Achieng pia walikamatwa wakati wa msako huo.
Msako huo pia ulitekelezwa kwenye nyumba iliyo karibu inayoaminika kuwa hifadhi katika sehemu hiyo hiyo ambako vifaa vya pimaji wa kimaabara, mashine ya dijitali ya kupima uzani na kitambulisho cha Curtis Muli zilipatikana.