Home Kimataifa Polisi wanasa bangi ya thamani ya shilingi milioni moja Kiambu

Polisi wanasa bangi ya thamani ya shilingi milioni moja Kiambu

0

Maafisa wa polisi katika eneo la Gatundu jana Jumatano walinasa bangi ya thamani ya shilingi milioni moja iliyokuwa imepandwa katika shamba la kibinafsi.

Maafisa hao ambao walikuwa wamepashwa habari, walivamia shamba hilo na kupata bangi hiyo ikiwa imepandwa pamoja na mimea mingine.

Kulingana na afisa mkuu wa polisi wa kaunti ndogo ya Gatundu Ellen Wanjiku, mimea 500 ya bangi ilinaswa katika shamba hilo ambalo pia lilikuwa na mahindi.

Wanjiku aliwaambia wanahabari kwamba kunaswa kwa bangi hiyo ni sehemu ya mpango unaolenga kutokomeza mihadarati na pombe haramu katika eneo hilo.

Wakati wa msako huo ulioongozwa na maafisa wa polisi kutoka Gatundu Kaskazini na Thika, machifu na manaibu wao, washukiwa watatu walikamatwa na kupelekwa katika kituo cha polisi cha Mwea ili kuhojiwa.

Kwa upande wake, kamanda wa polisi wa kaunti ndogo ya Thika Magharibi Moses Sirma alisema maafisa wa polisi wameongeza misako yao ili kusambaratisha shughuli zote haramu katika eneo hilo.

Website | + posts