Maafisa wa polisi wa kukabiliana na uhalifu wa jinai DCI, wanamtafuta mwanamke wanayemshuku alihusika katika mauaji ya kinyama ya daktari Erick Maigo, aliyekuwa kaimu Mkurugenzi wa fedha katika Nairobi hospital.
Kupitia mtandao wa X awali twitter, idara ya DCI ilitoka wito kwa wananchi kutoa habari kumhusu mwanamke ambaye picha yake ilinakiliwa na kamera fiche za CCTV akitoka katika nyumba ya Maigo kupitia mlango wa nyuma.
“Kufuatia mauaji ya kinyama ya Dkt. Erick Maigo, maafisa wa DCI wanatoa wito kwa wananchi kutoa habari zitakazofanikisha kuitiwa nguvuni kwa mwanamke huyo,” ilisema taarifa ya DCI.
Visu viwili vilivyokuwa na damu vinavyoaminika kutumiwa katika mauaji hayo, vilipatikana katika eneo la mkasa.
Mwili wa Dkt. Maigo ulipatikana nyumbani kwake tarehe 15 mwezi Septemba asubuhi ukiwa na majeraha ya kudungwa kisu.