Home Habari Kuu Polisi wamuua mshukiwa wa mauaji ya afisa wa polisi David Mayaka

Polisi wamuua mshukiwa wa mauaji ya afisa wa polisi David Mayaka

Bastola iliyotumika kumuua afisa Mayaka wiki mbili zilizopita, pia ilipatikana wakati wa oparesheni hiyo.

0

Mmoja wa washukiwa anayehusishwa na mauaji ya afisa wa polisi wa kitengo cha DCI David Mayaka ameuawa kwa kupigiwa risasi katika mtaa wa Kayole jijini Nairobi.

Inasemekana mshukiwa huyo kwa jina John Kamau, almaarufu  Farouk, alikataa kujisalimisha na badala yake akamfyatulia risasi mmoja wa maafisa waliokwenda kumtia nguvuni.

“Akiwa amejihami kwa bastola aina ya CZ, iliyofyatua risasi iliyomuua afisa Mayaka, jambazi huyo alitoka katika nyumba moja mtaani Njiru na kumfyatulia risasi mmoja wa maafisa wetu na kumjeruhi mguuni,” ilisema sehemu ya taarifa ya DCI.

Mshukiwa huyo alifumaniwa katika operesheni iliyotekelezwa na maafisa wa kikosi maalaum kutoka DCI katika nyumba yake mtaani Soweto.

Bastola iliyotumika kumuua afisa Mayaka wiki mbili zilizopita, pia ilipatikana wakati wa operesheni hiyo. Bastola hiyo ilikuwa na risasi 12.

Simu zinazoshukiwa kuwa ziliibwa kwa mabavu jijini Nairobi pia zilipatikana.

Uchunguzi wa maafisa wa polisi unaashiria kuwa bastola hiyo, imetumika katika visa vya wizi katika kaunti za Kiambu na Nairobi katika muda wa mwaka mmoja uliopita.

Visa hivyo vya wizi vililenga maduka ya MPESA katika mitaa ya  Kayole, Buruburu, Dandora na Dagoretti.

Kulingana na maafisa wa polisi, bastola hiyo iliibwa kutoka kwa mlinzi wa aliyekuwa Waziri mnamo mwaka 2921 katika kaunti ya Kajiado.

Wakati wa kisa hicho, mlinzi hiyo alikuwa akiingia nyumbani kwake mwendo wa saa nane usiku, alipofumaniwa na majambazi wanne wakiwa wamejihami kwa bunduki aina  AK-47 na vifaa butu.

Juma lililopita, polisi walimtia nguvuni mshukiwa mkuu katika mauaji ya afisa Mayaka na kunasa pikipiki iliyotumiwa katika mauaji hayo.

Msako dhidi ya mshukiwa wa tatu Henry Njihia, anayeaminika kuwa amejihami, unaendelea.

Afisa Mayaka ambaye alikuwa afisa wa DCI kituo cha  Makadara  alikuwa akielekea nyumbani akiwa na mkewe Kemunto Mayaka Agosti 8, saa nne usiku, alipovamiwa na majambazi.

Website | + posts

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here