Huduma ya Taifa ya Polisi chini ya uongozi wa kaimu Inspekta Mkuu Gilbert Masengeli imeshiriki tamasha kwa jina “Harmony4Haiti” yaani “Maelewano kwa ajili ya Haiti” katika bustani ya Uhuru Gardens, Nairobi.
Wakati wa tamasha hilo, Masengeli alikuwa ameandamana na kamanda wa kitengo cha GSU Ranson Lolmodooni, kamanda wa polisi katika eneo la Nairobi Adamson Bungei na msemaji wa polisi Resila Onyango.
Maafisa wa polisi wa Kenya walitumwa nchini Haiti mwezi Juni mwaka huu wa 2024 kufuatia kupitishwa kwa azimio la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa nambari 2699 la mwaka 2023.
Azimio hilo liliidhinisha kutumwa nchini Haiti kwa kikosi cha polisi kinachoongozwa na Kenya kusaidia polisi wa Haiti kukabiliana na magenge yenye silaha.
Kufikia sasa, kikosi hicho kimefanikiwa kurejesha kwa serikali miundombinu kadhaa kama vile uwanja wa ndege, bandari, hospitali ya kitaifa, chuo cha mafunzo kwa polisi na ikulu.
Magenge hayo yalikuwa yakidhibiti maeneo hayo.
Hali ya kawaida inaripotiwa kuanza kurejea nchini Haiti kwani sasa hata safari za ndege zimerejelewa.
Waziri aliye na Mamlaka Makuu Musalia Mudavadi ambaye alihudhuria tamasha hilo, aliwapongeza polisi kwa kujitolea kusaidia raia wa Haiti.
Mudavadi ameyaomba mataifa mengine kutoa mchango wa maafisa wa polisi na hata wa kifedha.