Home Habari Kuu Polisi Pokot Magharibi wanasa risasi 749, washukiwa watoroka

Polisi Pokot Magharibi wanasa risasi 749, washukiwa watoroka

0

Polisi katika kaunti ya Pokot Magharibi wamenasa risasi 749 zinazotumiwa katika bunduki aina ya AK47. 

Pokot Magharibi ni miongoni mwa kaunti za kaskazini mwa nchi ambazo zimeshuhudia visa vya ukosefu wa usalama kwa muda na msako mkali wa kuwasaka wahalifu umepamba moto.

Katika kisa cha hivi karibuni, risasi hizo zilinaswa kwenye kizuizi cha barabara cha Marich kwenye barabara kuu ya kutoka Kitale-Lodwar majira ya saa tisa alfajiri leo Jumanne.

Washukiwa wawili waliokuwa wanazisafirisha walikwepa walipofumaniwa na maafisa wa usalama na msako wa kuwatafuta umeshika kasi.

Washukiwa walikuwa wakisafiria kwenye pikipiki kuelekea upande wa Lodwar kutoka Kitale wakati risasi hizo zikiwa zimewekwa kwenye gunia.

Kamanda wa Polisi katika kaunti ya Pokot Magharibi Peter Katam alithibitisha kisa hicho.

Alisema bado hawana ufahamu ikiwa risasi hizo zilikuwa zikisafirishwa kuelekea kwenye mpaka wa Pokot Magharibi -Turkana au ule wa Pokot Magharibi, Elgeyo Marakwet  na Baringo.

Katam alisema msako dhidi ya silaha utaendelea hadi wahakikishe hamna silaha zozote  katika eneo hilo akiongeza kuwa dhamira ya serikali ni kuhakikisha visa vya ukosefu wa usalama vinakomeshwa.

Aliwataka wakazi kutohofia kwa kuripoti watu wanaowashuku kwa maafisa wa polisi na kuwahakikishia kuwa usalama umeimarishwa.

Alitaja unasaji wa risasi hizo kuwa mafanikio makubwa kwa vita dhidi ya ufisadii.

Kadhalika alitoa wito kwa wale wanaomiliki silaha kinyume cha sheria kuzisalimisha.

Msako wa kuwatafuta washukiwa waliotorokea kwenye giza totoro lililofunika anga wakati huo unaendelea.

Martin Mwanje & Stephen Aengwo
+ posts