Home Habari Kuu Polisi Kiambu wanasa kemikali ya Ethanol

Polisi Kiambu wanasa kemikali ya Ethanol

Maafisa wa polisi wa eneo la Juja katika kaunti ya Kiambu wamenasa lita 8,750 za kemikali ya Ethanol, katika kijiji cha Mugutha.

Kemikali hiyo ambayo ni kiungo cha kutengeneza pombe, ilinaswa baada ya wakazi kutoa habari kwa polisi kuhusu vitendo vya kushukiwa katika jengo husika hasa nyakati za usiku.

Jengo hilo ambapo kemikali hiyo ya Ethanol ilipatikana ikiwa imepakiwa katika mitungi 35 ya lita 250 awali lilikuwa kiwanda cha macadamia ambacho kiliacha kutumika.

Kulingana na kamanda wa polisi katika kaunti ya Kiambu Michael Muchiri, Ethanol hiyo lita 8,750 inatosha kutengeneza pombe ya thamani ya shilingi milioni 70.

Kitu kingine kilichopatikana humo ni tangi kubwa la maji ambalo polisi wanachunguza ili kubaini iwapo lilikuwa likitumika kuunda pombe.

Lori linaloshukiwa kutumika kusafirisha bidhaa hadi eneo hilo na kutoka eneo hilo pia lilipatikana na Muchiri alisema kwamba oparesheni yao imelinda wakazi wa eneo hilo dhidi ya matumizi ya pombe haramu ambayo haijatimiza viwango na ni sumu.

Anahisi wanaoendesha shughuli katika eneo ambako Ethanol ilipatikana huenda wakawa wahalifu wanaosaidia kuunda pombe mbaya ambayo imekuwa ikilaumiwa kwa kudhuru watumiaji.

Hata ingawa hakuna aliyekamatwa kwenye oparesheni hiyo, mkubwa huyo wa polisi amefichua kwamba maafisa wa upelelezi wanafuatilia taarifa muhimu ili kuhakikisha wahusika wanakamatwa.

Alisema polisi wataendeleza oparesheni dhidi ya pombe haramu ili kulinda wakenya. Aliomba wakenya kutoa habari kuhusu utengenezaji na uuzaji wa pombe aina hiyo.