Maafisa wa polisi katika kaunti ya Makueni jana walikamata magari mawili yaliyokuwa yamebeba nyama inayodhaniwa kuwa ya punda iliyokuwa ikisafirishwa kuelekea Nairobi, hususan soko la Shauri Moyo.
Kulingana na taarifa ya polisi kwenye akaunti yao ya mtandao wa X magari hayo ni aina ya Toyota Fielder nambari ya usajili KDB 991U na Toyota Wish nambari KCK 434M.
Washukiwa kumi ambao ni Antony Kiiru, Samson Kamau, Paul Kabura, Cyrus Nthumbi, Isaac Njoroge, Johnstone Kilunja, Samuel Mwangi, Andrew Kithiki, Carol Makau na Francis Makau walikamatwa.
Baadaye washukiwa hao waliongoza kundi la maafisa wa polisi na wa afya ya umma hadi eneo ambalo huwa wanachinjia wanyama hao ambalo ni makazi ya mmoja wao.
Katika boma hiyo walifukua vichwa vya punda 25 pamoja na kwato za punda. Maafisa hao walipata pia vifaa ambavyo vinaaminika kutumika kuchinja punda hao.
Biashara ya nyama ya punda ilihalalishwa nchini Kenya mwaka 2012 lakini ulaji wa nyama hiyo haujakita mizizi bado.
Hata hivyo nyama yoyote ya kuuzwa inastahili kutoka kwenye vichinjio halali vilivyoidhinishwa na maafisa wa afya ya umma na kusafirishwa kwenye magari maalum yaliyoidhinishwa.