Home Habari Kuu Polisi hawatahudumu kituo kimoja zaidi ya miaka 3, asema Kindiki

Polisi hawatahudumu kituo kimoja zaidi ya miaka 3, asema Kindiki

0

Hakuna afisa yeyote wa polisi atakayeruhusiwa kuhudumu katika kituo kimoja zaidi ya miaka mitatu. 

Agizo hilo, ambalo ni sehemu ya mapendekezo ya Jopokazi juu ya Mabadiliko katika Idara ya Polisi lililoongozwa na Jaji Mkuu Mstaafu David Maraga, limetolewa na Waziri wa Usalama wa Kitaifa Prof. Kithure Kindiki.

Prof. Kindiki ameipa Huduma ya Kitaifa ya Polisi, NPS siku 60 kulitekeleza.

“Mshahara wa afisa yeyote asiyetii agizo hilo baada ya siku 60 utasimamishwa mara moja,” alionya Prof. Kindiki alipofika katika bunge la Seneti leo Jumatano kujibu maswali mbalimbali kutoka kwa Maseneta kuhusiana na usalama wa kitaifa.

Agizo hilo limetolewa wakati ambapo kumekuwa na vilio vya mara kwa mara kutoka kwa raia vya kutaka maafisa kadhaa wa polisi kuhamishwa kutoka vituo mbalimbali nchini kutokana na utepetevu wanaodai unatokana na wao kuhudumu katika vituo hivyo kwa muda mrefu.

Na ili kuimarisha usalama na kuwawajibisha wanaoendelea uhalifu kama vile utekaji nyara, Waziri huyo alisema serikali inaimarisha doria, kuhamasisha jamii kuhusu umuhimu wa kushirikishana taarifa za kijasusi kuhusu watu wanaowashuku sehemu wanakoishi na ambao huenda wakatekeleza uhalifu.

Aidha mpango wa Nyumba Kumi unaolenga kuimarisha usalama vijijini nao unaboreshwa.

Awali, Prof. Kindiki aliwaambia Maseneta hao kuwa nyadhifa zote zilizo wazi za Machifu na Manaibu wao zitajazwa ndani ya siku 90 zikihusisha zile ambazo mchakato wa kuwahoji watu wa kuzijaza tayari umekamilika.

Anasema kuna mipango ya kuwaajiri na kuwapeleka Machifu na Manaibu wao kujaza nyadhifa zilizo wazi katika maeneo mbalimbali nchini.

“Nyadhifa hizo zilisalia wazi kutokana na vifo, kufutwa kazi kwa maafisa baada ya kesi zao kukamilika mahakamani au kushughulikiwa na Tume ya Utumishi wa Umma na hakuna rufaa iliyowasilishwa mahakamani, kupandishwa vyeo kwa maafisa waliohudumu katika nyadhifa hizo, kujiuzulu au maafisa kukabidhiwa majukumu mapya,” alisema Waziri Kindiki.

Kuna jumla ya kata 3,955 na kata ndogo 9,045 kote nchini zinazohudumiwa na Machifu na Manaibu wao, na serikali inalenga kujaza nyadhifaa zilizosalia wazi katika hatua inayolenga kuimarisha usalama kila pembe ya nchi.

 

Website | + posts