Home Michezo Paul Pogba: Kiungo wa Juventus asimamishwa kwa kosa la kutumia dawa za...

Paul Pogba: Kiungo wa Juventus asimamishwa kwa kosa la kutumia dawa za kusisimua misuli

0

Kiungo wa Juventus Paul Pogba amesimamishwa kwa muda kutocheza kwa sababu ya kosa la matumizi ya dawa za kusisimua misuli.

Mahakama ya kitaifa ya kupambana na dawa za kusisimua misuli ya Italia (Nado) ilisema kuwa Pogba alirejesha kipimo cha testosterone baada ya ushindi wa 3-0 wa Juve dhidi ya Udinese mnamo tarehe 20 Agosti.

Mchezaji wa kimataifa wa Ufaransa Pogba, 30, alikuwa mchezaji wa akiba ambaye hatumiwi lakini alichaguliwa kwa bahati nasibu kwa ajili ya uchunguzi baada ya mechi.

Iwapo atapatikana na hatia ya kutumia dawa za kusisimua misuli, anaweza kupigwa marufuku kati ya miaka miwili na minne.

Juventus ilisema katika taarifa: “Klabu ya Soka ya Juventus inatangaza kwamba leo, 11 Septemba, 2023, mchezaji wa mpira wa miguu Paul Labile Pogba alipokea agizo la kusimamishwa kwa tahadhari kutoka kwa Mahakama ya Kitaifa ya Kupambana na Dawa zinazopigwa marufuku michezoni baada ya matokeo ya vipimo vilivyofanywa tarehe 20 Agosti, 2023.

“Klabu inazingatia hatua zinazofuata za kiutaratibu.”

Nado imesema Pogba alikiuka sheria za kupinga matumizi ya dawa za kusisimua misuli walipopata dutu iliyopigwa marufuku “metaboli za testosterone zisizo asilia”

Testosterone ni homoni ambayo huongeza uvumilivu wa wanariadha.

Pogba ana siku tatu kufanya uchambuzi wa kupinga matokeo kwa Nado.Juventus ilimsajili tena Pogba kwa mkataba wa miaka minne Julai 2022 baada ya mchezaji huyo kumaliza mkataba wake na Manchester United na kuondoka kama mchezaji huru.

Hata hivyo, kurejea kwa Pogba Turin kumekumbwa na matatizo ya mara kwa mara ya majeraha ambayo pia yalimfanya kukosa Fainali za Kombe la Dunia mwaka jana nchini Qatar.

Pogba amecheza jumla ya dakika 51 kama mchezaji wa akiba msimu huu katika mechi na Bologna na Empoli.

Msimu uliopita alicheza kwa dakika 108 katika mechi sita za Serie A, mechi tatu fupi na asisti moja kwenye Ligi ya Europa, na dakika 11 kwenye Coppa Italia – jumla ya dakika 162 bila bao.

Matatizo ya jeraha ya Pogba yalianza tena hivi karibuni, huku kocha wa Juventus Massimo Allegri akisema mchezaji huyo alipata tatizo dogo la mgongo baada ya mechi dhidi ya Empoli.

BBC
+ posts