Home Habari Kuu Passaris apokelewa visivyo na waandamanaji Nairobi

Passaris apokelewa visivyo na waandamanaji Nairobi

0

Mwakilishi wa kike wa kaunti ya Nairobi bungeni Esther Passaris jana alijipata pabaya alipojaribu kujiunga na maandamano ya kupinga mauaji ya wanawake Nairobi.

Passaris alijiunga na maandamano hayo baada ya muda na waandamanaji walikuwa macho kuona namna viongozi watachukulia maandamano yenyewe.

Alipojaribu kuwahutubia waandamanaji katika bustani ya Jevanjee, kiongozi huyo alipigiwa kelele akiulizwa alikokuwa mauaji hayo yakitokea na kutakiwa arejee nyumbani.

Analaumiwa kwa kutosema lolote na kutochukua hatua kuhusu mauaji ya wasichana wawili katika eneo analowakilisha.

Esther hata hivyo hakufa moyo na aliendelea na maandamano kama wengine kwenye sehemu mbali mbali za jiji la Nairobi.

Baadaye akizungumza na wanahabari, alielezea kwamba alikuwa mmoja wa waliopanga na kufadhili maandamano hayo ya kupinga mauaji ya kiholela ya wanawake.

“Ninaelewa kuna hasira nyingi lakini kuielekeza kwa kiongozi wa kike sio jambo zuri” alisema Passaris akiongeza kwamba uwajibikaji unaanza kutoka juu kabisa serikalini.

Alionyesha kutoridhika kwake na hatua ya kuzuiwa asihutubie waandamanaji hao akisema yeye ni mwanamke, ana binti na hakufurahia kusikia wanawake wanauawa ovyo.

Maandamano hayo yalipangwa na makundi mbali mbali ya kutetea haki za binadamu na yale ya wanaharakati kufuatia kuuawa kwa wanawake na watu wanaojisingizia kuwa wateja wao.

Lengo kuu ni kushinikiza serikali kuchukua hatua kuzuia matukio kama hayo siku za usoni.

Website | + posts