Home Burudani Pallaso asema tamasha la London litafana hata bila yeye

Pallaso asema tamasha la London litafana hata bila yeye

0

Mwanamuziki wa Uganda Pius Mayanja au ukipenda Pallaso amesema kwamba tamasha ambalo alikuwa amepangiwa kuhudhuria jijini London, Uingereza kama mmoja wa watumbuizaji litakuwa zuri hata bila uwepo wake.

Kaka huyo wa Jose Chameleone aliondolewa kwenye orodha ya watumbuizaji baada ya hasimu wake Alien Skin kutishia kujiondoa iwapo Palasso atakuwepo.

Pallaso alistahili kutumbuiza kwenye tamasha la Purple Party Juni 24, 2023, ndani ya ukumbi wa Royal Regency pamoja na Alien Skin, Azawi, David Lutalo na Mikie Wine kati ya wasanii wengine.

Hatua ya kumwondoa dakika za mwisho mwisho anasema ni jaribio kubwa kwake na watu wake lakini watasalia wajasiri.

Alien alisema jana kwamba hataonekana jukwaani iwapo Pallaso angetumbuiza kwenye tamasha hilo kwani hakuwa na lolote la kuhakikishia umma.

Inasemekana waandalizi waliamua kumchuja Pallaso kufuatia tukio ambapo alionekana akimzaba Alien kofi hadharani baada ya majibizano.

Pallaso ametumia mitandao ya kijamii kuonyesha kutoridhika kwake na hatua iliyochukuliwa na waandalizi wa tamasha hilo huku akiomba mashabiki wake msamaha.

Ameashiria kwamba waandalizi tofauti wa matamasha wamewasiliana naye ili kumwandalia tamasha jingine na atajuza mashabiki iwapo wataafikiana.

Website | + posts