Home Kimataifa Owalo akutana na mwenyekiti mpya wa bodi ya KBC

Owalo akutana na mwenyekiti mpya wa bodi ya KBC

0
kra

Waziri wa Habari, Mawasiliano na Uchumi wa Dijitali Eliud Owalo leo Jumatatu asubuhi alikutana na Tom Mshindi ambaye ni mwenyekiti mpya wa bodi ya shirika la utangazaji nchini, KBC. 

Wakati wa mkutano huo, Owalo anasema walizungumzia mikakati ya kulifufufua shirika hilo, ikiwa ni pamoja na hatua zinazopaswa kuchukuliwa sasa na zile za muda mrefu.

kra

“Namshukuru Rais William Ruto kwa kumteua mwanahabari anayeheshimiwa, mwenye tajriba na uzoefu wa muda mrefu kupiga jeki juhudi za kulihuisha shirika la KBC,” alisema Owalo baada ya mkutano huo.

Ijumaa iliyopita, Rais Ruto alimteua Mshindi kuwa mwenyekiti mpya wa bodi ya shirika la KBC kwa kipindi cha miaka mitatu.

Kupitia kwa gazeti rasmi la serikali, Ruto alifutilia mbali uteuzi wa mhandisi Benjamin Maingi kuwa mwenyekiti wa bodi hiyo.

“Kwa mujibu wa mamlaka niliyo nayo kupitia sehemu ya 7 (3)  ya sheria za shirika la utangazaji nchini…namteua Tom Mshindi Nyamancha kuwa mwenyekiti wa bodi ya shirika la utangazaji nchini, KBC kwa kipindi cha miaka mitatu, kuanzia Januari 19, 2024,” alisema Rais Ruto kupitia gazeti hilo.

Tom Mshindi alihitimu kutoka Chuo Kikuu cha Nairobi, ambako alisomea uanahabari, kabla ya kufanya kazi katika vituo mbalimbali vya habari hapa nchini.

Mshindi pia aliwahi kuwa mhariri katika shirika la umoja wa mataifa la kuwahudumia watoto, UNICEF jijini New York nchini Marekani.

Website | + posts