Home Habari Kuu Oparanya: Hakuna migawanyiko katika chama cha ODM

Oparanya: Hakuna migawanyiko katika chama cha ODM

Oparanya alitaja madai hayo kuwa uvumi unaoenezwa na maadui wa chama hicho.

0

Naibu kiongozi wa chama cha Orange Democratic Movement (ODM) Wycliffe Oparanya, amepuuzilia mbali madai kwamba kuna migawanyiko katika chama hicho.

Akizungumza na wanahabari baada ya kumtembelea gavana wa Busia Paul Otuoma afisini mwake, Oparanya alitaja madai hayo kuwa uvumi unaoenezwa na maadui wa chama hicho.

“Hakuna swala kama hilo, chama cha ODM kiko imara, labda kuna watu wanajitafutia sifa kwa kusema kuna migawanyiko chamani,” alisema Oparanya.

Kulingana na Oparanya, hakuna mwanachama yeyote wa ODM amezindua kampeni za kisiasa kwa kuwa zoezi la kuwaandikisha wananchama mashinani bado linaendelea.

“Kampeini haziwezi kutekelezwa hadi wakati uchaguzi wa mashinani utakapoandaliwa,” aliongeza gavana huyo wa zamani wa Kakamega.

Aidha alisema kwa kuwa kiti cha kiongozi wa chama hicho Raila Odinga hakiko wazi, hakuna mwanachama atajihusisha na siasa za urithi.

“Swala la Raila kuchaguliwa katika tume ya Umoja wa Afrika, litatekelezwa katika muda wa mwaka mmoja ujao, tutajadiliana vipi kuhusu kumrithi Raila akiwa angali katika uongozi wa ODM?,” aliuliza Oparanya.

Kwa upande wake, Gavana wa Busia Paul Otuoma, alisema ni mapema sana kujihusisha na siasa za kumrithi kiongozi wa chama hicho akiwa bado mamlakani.

“Viongozi wa chama wanapaswa kujihusisha na kuwaandikisha wanachama kabla ya chaguzi za mashinani mwezi Aprili mwaka huu,” alisema Otuoma.

Otuoma aliongeza kuwa chama cha ODM kiko imara na kitaendelea kuwa imara katika eneo la kaskazini mwa nchi.