Home Michezo Omanyala kuongoza Kenya kusaka tiketi ya Olimpiki

Omanyala kuongoza Kenya kusaka tiketi ya Olimpiki

0

Kenya italenga tiketi ya Olimpiki itakaposhiriki makala ya sita ya mbio za kupokezana virojo duniani baina ya kesho na Jumapili mjini Nassau,Bahamas.

Kenya inajivunia kikosi dhabiti cha mbio za mita 100 kwa wanariadha wanne kupokezana na mita 400 kwa wanariadha wanne kupokezana huku timu 14 bora, katika mashindano hayo zikifuzu kwa michezo ya Olimpiki itakayoandaliwa Paris Ufaransa kati ya Julai 26 na Agosti 11.

Mwanariadha mwenye kasi barani Afrika katika mbio za mita 100 Ferdinand Omanyala ataongoza kikosi cha mita 100 kinachowajumuisha Mark Otieno,Samuel Waweru,Hesbon Ochieng, Mike Mokamba,na Meshack Babu.

Timu ya Kenya katika mbio hizo inaorodheshwa ya 38 duniani, huku ile ya mita 400 ikishikilia nafasi ya 50 kwenye msimamo wa dunia.

Timu 14 bora zitafuzu kwa moja kwa moja kwa michezo ya Olimpiki .

Afisa wa kamati kuu ya chama Riadha Barnaba Korir, amesema wana imani ya kufuzisha timu za Kenya kwa michezo ya Olimpiki kupitia kwa mashindano hayo ya Bahamas.

Boniface Mweresa,Wiseman Were,Zablon Ekwam, na Moitalel Mpoke wataongoza kikosi cha moita 400 wanaume kupokezana virojo.

Timu ya wanawake ya mita 400 kwa wakimbiaji wanne kupokezana kijiti ya wanawake itakuwa na kibarua kigumu kufuatia kujiondoa kwa bingwa wa dunia Mary Moraa na inasalia na Vanice Kerubo,Joan Cherono,Rahab Wanjiru,Jackline Nanjala, Veronicah Mutua na Diana Chebet.

Mashindano ya Bahamas yatashirikisha awamu za kufuzu kwa Olimpiki kabla ya fainali Jumatatu Alfajiri.

Kenya ilitwaa medali mbili za shaba katika mbio za mita 200 kwa wanariadha wanne kupokezana virojo kwa wanaume na wanawake mwaka 2021 mjini Silesia Poland .

Website | + posts