Home Habari Kuu Okwaro ataka mashauriano kati ya serikali na upinzani

Okwaro ataka mashauriano kati ya serikali na upinzani

Okwaro amewarai washirika wa karibu wa Rais William Ruto na wa kiongozi wa Upinzani Raila Odinga kulegeza misimamo ili kuruhusu mazungumzo.

0

Katibu Mkuu wa muungano wa wafanyakazi katika sekta ya mawasiliano nchini Benson Okwaro ametaka kuandaliwa kwa majadiliano ya kina kati ya serikali na upinzani ili kumaliza maandamano ambayo yameathiri utendakazi na kudumaza uchumi.

Katika mahojiano ya kipekee na KBC, Okwaro amesema huenda maandamano yanayooitishwa na upinzani yakaathiri pakubwa utendakazi nchini na kusababisha uharibifu wa mali na maafa badala ya kutoa suluhisho kwa changamoto zinazowakumba Wakenya.

“Itakuwa bora kama serikali na upinzani watajadiliana changamoto zonazowakumba Wakenya ikiwemo gharama ya juu ya maisha badala ya maandamano ambayo naamini hayatatoa suluhu yoyote, “alisema Okwaro.

Okwaro ambaye pia ni Naibu Katibu Mkuu wa Muungano wa Wafanyakazi Nchini, COTU amewarai washirika wa karibu wa Rais William Ruto na wa kiongozi wa upinzani Raila Odinga kulegeza misimamo ili kuruhusu kufanyika kwa mazungumzo.

“Tatizo kubwa ambalo tunaona ni wandani wa Rais Ruto na wale wa Raila kuwa na misimamo mikali ambayo inafanya mazungumzo kuwa magumu na yote ni kwa sababu za kibinafsi,” aliongeza Okwaro.

“Tunawaomba kwa sababu ya kutaka Kenya isonge mbele na wafanyakazi wawe na mazingira bora ya kufanya kazi walegeze misimamo ili mazungumzo yafanyike.”

Matamshi ya Okwaro yanajiri wakati kumekuwa na hatihati kuhusu kuwepo kwa mazungumzo kati ya serikali na upinzani huku miito hiyo ikiongezeka kila kuchao kutoka lwa viongozi wa kidini.

Website | + posts

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here