Home Habari Kuu ODM yatangua uteuzi wa Wawakilishi Wadi 4 bunge la kaunti ya Kisumu

ODM yatangua uteuzi wa Wawakilishi Wadi 4 bunge la kaunti ya Kisumu

0

Chama cha ODM kimeendeleza hujuma dhidi ya wanachama wake wanaochukuliwa kuwa wanakiuka itikadi za chama na wameonyesha chembe za kukosa nidhamu.

Leo Alhamisi, imebainika kuwa chama hicho kimetangua uteuzi wa Wawakilishi Wanne wa chama hicho katika bunge la kaunti ya Kisumu.

Uamuzi huo ulifikiwa wakati wa mkutano wa Kamati Kuu ya Kitaifa ya chama hicho ulioandaliwa jana Jumatano.

Taarifa kutanguliwa kwa Wawakilishi Wadi hao wanne wateule zilitangazwa na Spika wa bunge la kaunti ya Kisumu Elisha Jack.

Wawakilishi Wadi ambao uteuzi wao umetanguliwa ni Carolyne Opar, Keneddy Ajwang, Peter Obaso na Regina Kizito.

“Leo, karibu majira ya mchana, nilipokea barua kutoka kwa chama cha ODM yenye mintarafu ODM/2023/180/00 na iliyoandikwa Septemba 7, 2023. Barua hiyo inazungumzia azimio lililofanywa na Baraza Kuu la Kitaifa la chama la kubatilisha Wawakilishi Wadi wafuatao,” alisema Spika Elisha katika taarifa na kisha kuwataja kwa majina.

“Kwa mujibu wa barua hiyo, nawaarifu kuwa Wawakilishi Wadi waliotajwa wamepigwa marufuku kutekeleza majukumu yote ya bunge mara moja. Hii inamaanisha kamwe hawatashiriki shughuli zozote za bunge hili hadi maelekezo zaidi yatakapotolewa.”

Hatua hiyo ikija siku moja baada ya baraza hilo kuwatimua chamani wabunge watano wanaochukuliwa kuwa waasi.

Wao ni pamoja na Phelix Odiwuor wa Lang’ata, Seneta wa Kisumu Profesa Tom Ojienda, mbunge wa Gem Elisha Odhiambo, Gideon Ochanda wa Bondo na mbunge wa Suba  Kusini Caroli Omondi.

Baraza Kuu la Kitaifa la ODM limesema hatua hiyo ilitokana na utovu wa nidhamu na hulka ya wabuunge hao kukaidi msimamo wa chama.

Wabunge hao wamekuwa wakishirikiana na utawala wa Kenya Kwanza katika hatua wanayosema inalenga kuvutia maendeleo katika maeneo bunge yao ya uwakilishi.