Home Habari Kuu ODM yadai serikali inasita kuangazia suala la gharama ya maisha

ODM yadai serikali inasita kuangazia suala la gharama ya maisha

0

Chama cha ODM kimeisuta serikali kwa madai kuwa haijaonyesha nia bayana ya kushughulikia suala la kupanda kwa gharama ya maisha. 

Kupitia katibu wake Edwin Sifuna, chama hicho kinasema ingawa Wakenya wamezongwa na kusongwa na gharama ya maisha, utawala wa Kenya Kwanza umekuwa ukisita kuangazia suala hilo wakati Wakenya wengi tayari wanateseka.

“Gharama ya maisha ni mwiba kwa mamilioni ya Wakenya. Wakenya wanateseka na wanalazimika kustahimili makali ya ushuru wa juu wanaotozwa na utawala wa Kenya Kwanza,” alisema Sifuna katika taarifa baada ya mkutano wa wabunge wa chama hicho ulioandaliwa leo Ijumaa.

“Ingawa baadhi ya wanachama wetu wanashiriki mazungumzo ya kamati ya uwiano wa kitaifa katika ukumbi wa Bomas, tunalaani kusita kwa utawala wa Kenya Kwanza kuangazia suala la gharama ya maisha.  Punda alichoka kitambo sasa ameanguka.”

Suala la gharama ya maisha limetishia kusambaratisha utayarishaji wa ripoti ya mwisho ya kamati ya uwiano wa kitaifa na kulazimu pande zote mbili kusitisha utayarishaji wa ripoti hiyo ili kufanya mashauriano zaidi na viongozi wakuu wa mirengo hiyo.

Serikali ya Kenya Kwanza kwa upande wake inasema imeweka mikakati kabambe ya kushughulikia suala hilo ikitaja ugavi wa mbolea ya bei nafuu na mbegu kwa wakulima katika hatua inayolenga kuongeza uzalishaji wa chakula nchini.

““Hatupaswi kuangazia manufaa ya muda mfupi katika mitazamo yetu katika kushughulikia masuala mbalimbali,” alisema Rais William Ruto wakati akiwahutubia viongozi wakuu serikalini wakiwemo mawaziri na makatibu jana Alhamisi.

Ruto kadhalika alisema hatachukua njia rahisi na maarufu bali ile muhimu, jasiri na yenye kuleta mabadiliko.

Alikiri kuwa njia hii itafanya hali kuwa ngumu, lakini “hii itafanya nchi yetu kubadilika milele”.

 

 

 

Website | + posts