Home Habari Kuu Raila akosoa serikali ya Kenya Kwanza

Raila akosoa serikali ya Kenya Kwanza

0

Kiongozi wa muungano wa upinzani Azimio la Umoja One Kenya Raila Odinga ameikosoa serikali ya Kenya Kwanza kwa kile anachokitaja kuwa hatua ya kuteka idara ya mahakama na bunge.

Raila vile vile amekosoa asasi za serikali za bunge na idara ya mahakama kwa kukubali kutawaliwa akisema hatua hiyo ni kinyume cha katiba.

Kiongozi huyo wa ODM naendeleza ziara yake katika eneo la Pwani kwa lengo la kusajili wanachama zaidi wa chama hicho.

Akizungumza katika eneo la Magarini, Raila alisema mkutano kati ya Rais Ruto na Jaji Mkuu Martha Koome ni hatua ya uchoyo na iliyo kinyume cha demokrasia.

Kulingana naye, yanayoshuhudiwa sasa chini ya serikali ya Kenya Kwanza hayajawahi kutokea kwenye tawala za awali.

Alishangaa kwamba spika wa bunge la kitaifa Moses Wetang’ula alihusika ilhali katiba imeelezea bayana kuhusu uhuru wa asasi mbalimbali za serikali.

Raila alimalizia kwa kusihi wanachama wa ODM kuungana ili chama kisalie kuwa imara.

Waliohudhuria hafla hiyo katika kaunti ya Kilifi ni Magavana wa kaunti ya Kilifi Gideon Mung’aro na mwenzake wa Mombasa Abdulswamad Sharif Nassir na pia naibu kiongozi wa chama cha ODM Wycliffe Oparanya miongoni mwa viongozi wengine.

Marion Bosire na Dickson Wekesa
+ posts