Home Habari Kuu OCS wa Ruai akamatwa na EACC kwa kudai hongo kutokwa kwa watu...

OCS wa Ruai akamatwa na EACC kwa kudai hongo kutokwa kwa watu waliokamatwa bila hatia

0
kiico

Afisa anayesimamia kituo cha polisi cha Ruai Duncun Otieng, alikamatwa usiku na maafisa wa tume ya ya maadili na kupambana na ufisadi nchini EACC kwa kosa la kudai hongo kutoka kwa watu aliokuwa amefungua kwenye seli za kituo hicho cha polisi kabla ya kuwaachilia huru.

Watu hao walisingiziwa makosa ya kuwa walevi na kuvuruga amani.

Hatua ya maafisa wa EACC ilichochewa na malalamishi kutoka kwa jamaa za mmoja wa watu ambao walikuwa wamekamatwa na kuzuiliwa katika kituo cha polisi cha Ruai.

Inaripotiwa kwamba Ijumaa usiku maafisa kutoka kituo hicho cha polisi cha Ruai waliingia katika sehemu ya burudani kwa jina Fun City huko Utawala na kukamata waliokuwepo bila hatia yoyote.

Walipelekwa kwenye seli za kituo hicho cha polisi ambapo walisalia hadi Jumamosi asubuhi ambapo OCS aliwataka kutoa shilingi elfu 5 kila mmoja ili waachiliwe bila masharti.

Afisa huyo anasemekana kuwatishia kwamba iwapo wangekosa kulipa pesa hizo, wangeendelea kuzuiliwa wikendi nzima na Jumatatu washtakiwe kwa makosa ya kuwa walevi na kuvuruga amani.

Bwana Duncun Otieng anazuiliwa katika kituo cha polisi cha Kilimani ambapo anasubiri hatua zaidi dhidi yake kwa mujibu wa sheria.

Afisa mkuu mtendaji wa EACC Twalib Mbarak alithibitisha kutiwa mbaroni kwa OCS huyo akisema kwamba tume hiyo imekuwa ikipokea malalamishi sawia ambapo maafisa wasimamizi wa vituo vya polisi wanakamata raia hasa wa umri wa makamo na kudai hongo kutoka kwao ili wawaachilie huru.

Aliwataka maafisa hao wajiepushe na visa hivyo huku akielezea kwamba katika visa vingine, watu hutupwa kwenye seli bila kusajiliwa kwa makosa yoyote kwenye kitabu rasmi na baadaye kulazimishwa kutoa hongo ili kuwa huru.

Mbarak ameshukuru raia kwa kuendelea kuripoti visa hivyo vya unyanganyi wa polisi kwa EACC badala ya kukubali kutoa hongo na akasihi wakenya wote kukumbatia hali ya kutii sheria.

kiico