Hellen Obiri ndiye bingwa mpya wa mbio za New York City Marathon baada ya kuziparakasa kwa saa 2 dakika 27 na sekunde 23 Jumapili jioni nchini Marekani.
Obiri alistahimili upinzani mkali kutoka kwa Letesenbet Gidey wa Ethiopia na bingwa wa mwaka jana Sharon Lokedi, lakini alitimka na kuwaacha wenzake na kukata utepe wa kwanza.
Ulikuwa ushindi wa pili wa marathon kwa mwanajeshi huyo na pia nchini Marekani, baada ya kutwaa ubingwa wa Boston Marathon mwezi April mwaka huu.
Gidey alichukua nafasi ya pili kwa saa 2 dakika 27 na sekunde 29, huku Lokedi akiridhia nafasi ya tatu kwa saa 2 dakika 27 na sekunde 33.
Obiri na Sifan wamefunga msimu wa mbio sita kuu za marathon ulimwenguni katika nafasi ya kwanza wakizoa alama 50 kila mmoja na watagawana kitita cha shilingi milioni 60.
TamiraT Tola wa Ethiopia ameshinda mbio za wanaume kwa saa 2 dakika 4 na sekunde 58, akifuatwa na Mkenya Albert Korir kwa saa 2 dakika 6 na sekunde 57, huku Shura Kitata wa Ethiopia akiambulia nafasi ya tatu.