Rais William Ruto amevunja kimya chake kufuatia taarifa ambazo zimekumbana na pingamizi kali kwamba Tume ya Mishahara na Marupurupu, SRC imependekeza maafisa wa serikali kuongezwa mshahara.
Rais Ruto sasa ameitaka Wizara ya Fedha kufanyia mapitio arifa ya Gazeti Rasmi la serikali ya Agosti 9, 2023 iliyotolewa na SRC kwa kuzingatia kwamba Mswada wa Fedha 2024 umeondolewa na changamoto za kifedha zinazotarajiwa kushuhudiwa mwaka huu wa fedha.
Arifa ya SRC iliangazia mishahara na mafao ya maafisa wa serikali kuu na Bunge la Kitaifa na lile la Seneti.
“Rais amesisitiza kuwa huu ni wakati, kuliko wakati wowote ule, kwa viongozi wa serikali kuu na mihimili yote ya serikali kuishi kulingana na uwezo wao,” amesema Hussein Mohamed ambaye ni msemaji wa Ikulu ya Nairobi.
Haijabainika ikiwa kwa kufanya mapitio hayo, Wizara ya Fedha itapendekeza kupunguzwa kwa mishahara ya maafisa wa ngazi za juu serikalini wakiwemo wabunge, maseneta, mawaziri na makatibu wao.
Wakenya kwa muda sasa wamelalamikia mishahara minono wanayolipwa wabunge humu nchini wakiitaja kuwa chanzo cha changamoto za kifedha zinazoikabili nchi.
Isitoshe, aliyekuwa Seneta mteule Millicent Omanga ametaka mishahara ya wabunge kupunguzwa wala si kuongezwa.
“Ni usaliti kwa Wakenya kwa mishahara na mafao mengine ya maafisa wa serikali kuongezwa kwa wakati huu ambapo kuna shinikizo la mishahara hiyo kupunguzwa,” alisema Omanga ambaye aligombea wadhifa wa Mwakilishi wa Wanawake katika kaunti ya Nairobi wakati wa uchaguzi mkuu uliopita ingawa hakufanikiwa.
“Hatuwezi daima kuwachukulia Wakenya kuwa wajinga. Punguza, wala usiongeze. Hicho ndicho wanachokitaka Wakenya!!!.”