Home AFCON 2023 Nyangumi wa Cape Verde wang’ata Ghana AFCON

Nyangumi wa Cape Verde wang’ata Ghana AFCON

0

Cape Verde almaarufu Blue Sharks walijituma kiume na kuwaduwaza Ghana mabao 2-1 katika mechi ya kundi B ya kombe la AFCON iliyopigwa ugani Felix Houffet Boigny jana Jumapili usiku.

Sharks walitawala mechi hiyo kwa kipindi kirefu huku wakichukua uongozi kupitia kwa bao la kipindi cha kwanza lake Jamiro Monteiro, akiunganisha mpira uliotemwa na kipa wa Ghana Richard Ofiri.

Black Stars kutoka Ghana walirejea kipindi cha pili kwa matao ya juu huku Alexander Djiku akiwarejesha mchezoni akisaidiwa na Jordan Ayew.

Wakipiga mahesabu ya kunusuru alama moja, Black Stars walibumbuazwa na goli la ushindi kutoka kwa nguvu mpya wa nyangumi wa visiwani Cape Verde, Garry Rodrigues dakika ya 92 na kuwapa ushindi wa kihistoria.

Ghana wana shinikizo la kuishinda Misri katika mechi ya pili kundini, ili kufufua matumaini ya kufuzu raundi ya pili.

Kwa upande wa nyangumi, wanahitaji pointi moja pekee kutoka mechi mbili zilizosalia  kufuzu kwa mwondoano kama ilivyokuwa mwaka 2021.