Chama tawala nchini Uganda cha National Resistance Movement (NRM) kimetangaza nia ya kuwaajiri vijana 145,000 watakaolinda kura za Rais Yoweri Museveni.
Lengo ni kuzuia wizi wa kura hizo katika uchaguzi mkuu uliopangwa kufanywa nchini humo mwaka 2026.
Hii inafuatia shutuma za Rais Museveni dhidi ya chama cha National Unity Platform (NUP) kwamba kiliiba kura milioni moja katika uchaguzi uliopita kutokana na mfumo mbovu uliowaruhusu watu kadhaa kupiga kura zaidi ya mara moja.
Vijana wanaolengwa kuajiriwa kwa shughuli hiyo ni wale walio kati ya umri wa miaka 20 na 45.
Uganda inatarajiwa kuelekea kwenye debe mwaka 2026 huku Rais Museveni ambaye amekuwa mamlakani tangu Januari 26, 1986, akigombea muhula mwingine afisini.