Kiongozi wa upinzani Raila Odinga amekana madai ya kukutana na Balozi yeyote wa nchi ya kigeni nchini leo Ijumaa.
Hii ni baada ya madai kuchipuka kuwa Raila pamoja na kiongozi wa chama cha Wiper Kalonzo Musyoka walikutana na mabalozi wa nchi za kigeni katika mtaa wa Karen jijini Nairobi.
“Hivi sasa, nimekabwa na mafua ambayo yamenilazimisha kusitisha shughuli zote za umma na mikutano,” amesema Raila.
“Kwa hivyo sijafanya mkutano na Balozi yeyote wa nchi ya kigeni kama ilivyodaiwa katika baadhi ya vyombo vya habari.”
Licha ya kuitisha maandamano ya siku tatu, Raila, Kalonzo, Martha Karua na viongozi wengine wa Azimio hawajajitokeza kuungana na wafuasi wao kushiriki maandamano hayo.
Kulingana na Raila, Kalonzo amezuiwa nyumbani kwake mtaani Karen na alitembelewa na kiongozi wa wengi katika bunge la Taifa Opiyo Wandayi aliyekuwa ameandamana na mbunge wa zamani wa Ndaragwa Jeremiah Kioni.
Maandamano ya Azimio ambayo yamezongwa na vurugu tele tangu yalipoanza juzi Jumatano yanakamilika leo.
Haijabainika dira itakayochukuliwa na Wanaazimio baada ya maandamano hayo kuonekana kuzimwa na serikali.
Rais William Ruto alikuwa ameapa kuhakikisha hakuna maandamano yatakayokubaliwa nchini na ameonya kuwa serikali yake itatokomeza hulka ya kuvunja sheria bila kuadhibiwa.