Bingwa wa Jumuiya ya Madola Mary Moraa atashuka uwanja wa kitaifa wa riadha mjini Budapest nchini Hungary Ijumaa usiku katika nusu fainali ya mita 800.
Moraa ambaye ndiye Mkenya pekee aliyesalia shindanoni amejumuishwa katika mchujo wa tatu wa nusu fainali dhidi ya bingwa mtetezi Athing Mu wa Marekani.
Moraa anaorodheshwa wa kwanza ulimwenguni mwaka huu baada ya kusajili matokeo mazuri katika mashindano ya Diamond League atapambana na Prudence Sekgodiso wa Afrika Kusini, Halimah Nakaayi wa Uganda huku semi fainali hiyo ikianza saa nne kasrobo usiku.
Mashindano mengine ya kusisimua leo Ijumaa ikiwa siku ya saba ya mashindano hayo ni fainali za mita 200 kwa wanaume na pia wanawake.
Fainali ya mita 200 kwa wanawake itaanza majira ya saa nne na dakika 40 usiku ikiwakutanisha bingwa wa mita 100 Sha’ Carri Richardson wa Marekani, bingwa mtetezi Shericka Jackson wa Jamaica, Marie Jose Talou wa Ivory Coast na Mwingereza Dina ASHER-SMITH.
Fainali ya wanaume itaanza kitifua vumbi saa nne na dakika 50 usiku kwa saa za Afrika Mashariki ikiwa vuta ni kuvute kati ya bingwa wa dunia wa mita 100 aliye pia bingwa mtetezi Noah Lyles wa Marekani, wenzake Keneth Bednarek na Erriyon Knighton na Mwingereza Zharnel Hughes pamoja na chipukizi wa Botswana Letsile Tebogo.