Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, amekataa wito wa kusitishwa kwa muda mapigano katika mzozo na Hamas.
Akizungumza wakati wa hotuba yake kwa njia ya televisheni, Netanyahu alisema hatakubali hatua hiyo hadi mateka wa Hamas waliotekwa wakati wa shambulio lake dhidi ya Israel tarehe 7 Oktoba waachiliwe.
Alikuwa akizungumza muda mfupi baada ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Antony Blinken kusisitiza wito wa “kusitishwa kwa vita ” katika mzozo huo ili kuruhusu misaada zaidi katika Gaza. Blinken pia alisema kusitishwa kwa vita hivyo kwa muda kunaweza kuunda “mazingira bora ambayo mateka wanaweza kuachiliwa”.
Blinken alisema maelezo ya jinsi kusitishwa huko kwa vita kungefanya kazi yanaangaziwa na kwamba Israel ilikuwa na “maswali halali” kuhusu jinsi mipango hiyo itafanya kazi
Lakini Netanyahu alisema: “Israel inakataa usitishaji vita wa muda ambao haujumuishi kurejea kwa mateka wetu.”
Ingawa usitishaji vita rasmi kwa kawaida huwa ni mipango ya muda mrefu unaoruhusu wahusika kushiriki katika mazungumzo, mapumziko ya kibinadamu yanaweza kudumu kwa saa chache.