Home Burudani Nelly athibitisha kwamba wamerudiana na Ashanti

Nelly athibitisha kwamba wamerudiana na Ashanti

0

Wanamuziki Nelly na Ashanti wamerudiana tena. Nelly ambaye jina lake halisi ni Cornell Iral Haynes Jr ndiye alithibitisha hilo kwenye mahojiano.

Alikuwa akihojiwa na Rasheeda kwenye kipindi chake cha mitandaoni kwa jina “Boss Moves” ambapo aliulizwa iwapo wamerudiana na mpenzi wake wa awali Ashanti.

Nelly aliangua kicheko kisha akajibu, “Ndio tuko sawa sasa.”

Ashanti Shequoiya Douglas ambaye ana umri wa miaka 42 sasa na Nelly ambaye ametimiza umri wa miaka 48 waliwahi kuwa wapenzi kati ya mwaka 2002 na mwaka 2013, uhusiano ambao uliwafurahisha sana wapenzi wa muziki wa Hip Hop.

Baada ya kuachana Ashanti alisema alihisi kwamba Nelly alimsaliti bila kuelezea kwa undani. Mwaka 2010 kwenye mahojiano, Nelly alisema kwamba hakuwa tayari kuingia kwenye ndoa na Ashanti.

Alisema walikuwa tu marafiki na kwa wakati huo alikuwa akiangazia tu kazi yake kama mwanamuziki.

Disemba mwaka jana walipata fursa ya kutumbuiza pamoja jukwaani ambapo waliimba wimbo wao “Body on Me”. Wamekuwa wakionekana pamoja kwa muda wa mwaka mmoja sasa na kusababisha uvumi kuhusu kurejeleana kama wapenzi.

Kwenye mahojiano na Rasheeda, Nelly alisema kwamba kuachana kwao kuliwasaidia kila mmoja kujiboresha na sasa wameboreka kama wapenzi.