Mshambulizi matata wa Ufaransa Kylian Mbappe anasema ndoto yake imetimia baada ya uamuzi wake wa kujiunga na miamba wa soka barani Ulaya Real Madrid kuthibitishwa jana Jumatatu.
Mbappe amekuwa akisakata soka na timu ya Paris St-Germain almaarufu PSG na mkataba wake na timu hiyo utakamilika tarehe 30 mwezi huu.
Mchezaji huyo shupavu mwenye umri wa miaka 25 atahamia Uwanja wa Bernabeu kwa mkataba wa miaka mitano na atatia mfukoni yuro milioni 15 kila msimu kwa miaka mitano. Aidha, ataweka asilimia kubwa ya haki zake za picha.
“Hakuna mtu anayeweza kuelewa jinsi nimefurahi!” Mbappe alisema hayo kupitia kwenye Instagram.
“Ndoto yangu imetimia. Nina furaha na kujivunia kujiunga na klabu ya ndoto zangu.”
Atajiunga na timu ya Real Madrid ambayo iliibuka mabingwa wa ligi kuu ya Uhispania La Liga, huku wakiinua taji la 15 kwenye kombe la ubingwa barani Ulaya baada ya kupata ushindi dhidi ya Borussia Dortmund kwenye fainali ya kipute hicho.
Kuwasili kwa Mbappe katika mji mkuu wa Uhispania huenda ukafanya klabu ya Real Madrid kuzidi kuwa timu bora zaidi huko Uropa, kutokana na matarajio ya kusisimua ya yeye kujiunga na washambulizi wa Brazil Vinicius Jr, Rodrygo na mchezaji mwenzake Endrick na kiungo wa Uingereza, Jude Bellingham.
Mbappe ambaye alikuwa mchezaji wa klabu ya PSG huko Ufaransa, alikubali kujiunga na Real mwezi Februari na akatangaza kuwa atawaaga mabingwa hao wa Ufaransa msimu huu ukifika tamati. Anaondoka katika mji mkuu wa Ufaransa kama mfungaji bora zaidi wa PSG, akiwa na mabao 256 tangu ajiunge nao kutoka Monaco mwaka wa 2017. Mshambulizi huyo pia amekuwa mfungaji bora katika ligi kuu ya Ufaransa kwa miaka sita mfululizo.
Hata hivyo, mfaransa huyo bado hajawahi kufanikiwa kushinda kombe la ubingwa barani Ulaya, baada ya kushindwa kwenye fainali msimu wa 2019-2020, jambo ambalo anatarajia kurekebisha akiwa na klabu ya Real Madrid ambayo imekuwa na mazoea ya kushinda taji hilo na kuibuka timu bora zaidi Uropa.