Home Habari Kuu Ndindi Nyoro ajitenga na siasa za urithi

Ndindi Nyoro ajitenga na siasa za urithi

Nyoro alisema anawaheshimu Rais Ruto na naibu wake Gachagua, akidokeza kuwa wawili hao wanapaswa kuungwa mkono kutoka maeneo yote.

0
Mbunge wa kiharu Ndindi Nyoro.

Mbunge wa Kiharu Ndindi Nyoro, amejitenga na siasa za urithi zinazoendelea katika eneo la mlima Kenya, akisema anamuunga mkono kiongozi wa taifa Rais William Ruto na naibu wake Rigathi Gachagua.

Matamshi ya Nyoro yanajiri huku cheche za maneno kutoka baadhi ya viongozi wa eneo la Mlima Kenya zikisheheni, kuhusu ni nani anapaswa kumrithi naibu Rais Rigathi Gachagua katika uchaguzi Mkuu wa mwaka 2027.

Hata hivyo Nyoro alisema anawaheshimu Rais Ruto na naibu wake Gachagua, akidokeza kuwa wawili hao wanapaswa kuungwa mkono kutoka maeneo yote.

Seneta wa Nyeri Wamatinga Wahome na mwenzake wa Murang’a Joe Nyutu, wamekuwa katika mstari wa mbele kumpigia debe mbunge Ndindi Nyoro kumrithi naibu Rais Rigathi Gachagua katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2027.

Akizungumza siku ya Alhamisi katika kaunti ya Meru, Naibu Rais Rigathi Gachagua, aliwaonya maseneta hao dhidi ya kuzungumzia siasa za urithi za mwaka 2027, akitaja matamshi yao kuwa ya kiholela.

Badala yake, Rigathi aliwataka maseneta hao wawili kuzingatia maswala ya maendeleo badala ya siasa zisizokomaa.

Nyoro alikuwa akizungumza katika kijiji cha Kanyarkwat, kaunti ya Pokot Magharibi wakati wa mazishi ya mhubiri Mary Moroto, mke wa mbunge wa mbunge wa Kapenguria Dkt. Samuel Moroto, aliyefariki kutokana na saratani.