Home Kimataifa Nchi za Afrika zatetea wajumbe wengi waliohudhuria COP28

Nchi za Afrika zatetea wajumbe wengi waliohudhuria COP28

0
Rais wa Nigeria Bola Tinubu amehudhuria mkutano wa COP28 mjini Dubai

Serikali kadhaa za Afrika zinatetea uamuzi wa kupeleka jumbe mkubwa kwenye mkutano wa mabadiliko ya tabianchi COP28 mjini Dubai baada ya hatua hiyo kukosolewa vikali.

Orodha ya Umoja wa Mataifa ya waliohudhuria mkutano huo imebaini kuwa Nigeria, Morocco, Kenya, Tanzania, Ghana na Uganda ni miongoni mwa nchi zilizopeleka wajumbe wengi.

Nigeria ilipeleka watu 1,411, ikifuatiwa na Morocco 823, na Kenya 65.

Wawakilishi wa Nigeria na Kenya Jumapili walisema kwamba wajumbe wengi kwenye orodha zao hawakufadhiliwa na fedha za umma kwani walikuwa wakiwakilisha vyombo vya habari, mashirika ya kiraia na taasisi za kibinafsi.

Nchi zote mbili pia zilisema kuwa baadhi ya wajumbe walioorodheshwa wanashiriki kwa mbali.

“Kama nchi kubwa zaidi barani Afrika, yenye uchumi mkubwa na yenye mchango mkubwa katika hatua za tabianchi na nchi yenye uchumi mkubwa wa madini, ni jambo lisilopingika kwamba wajumbe kutoka Nigeria watakuwa wengi kuliko nchi nyingine yoyote barani Afrika,” taarifa ya mshauri wa Rais wa Nigeria Bola Tinubu ilisema.

Msemaji wa Ikulu ya Kenya Hussein Mohammed aliambia runinga ya kibinafsi ya Citizen kwamba idadi hiyo “ilitiwa chumvi” kwani inawakilisha wale waliojiandikisha kwa hafla hiyo – sio waliohudhuria.

Aliongeza kuwa serikali ya kitaifa ilikuwa na wajumbe muhimu 51 pekee na waliosalia wamefadhiliwa na makundi mengine.

Katika taarifa yake, serikali ya Tanzania imesema zaidi ya asilimia 90 ya wajumbe kutoka nchi hiyo wamefadhiliwa na sekta binafsi.