Chama cha Narc Kenya kimetoa ilani ya kuondoka katika muungano wa Azimio.
Narc Kenya pamoja na ODM, Wiper, DAP-K, Jubilee na PNU ni vyama tanzu vya muungano huo unaoongozwa na Raila Odinga.
Kimesema hatua hiyo imetokana na kuteuliwa kwa wanachama wa ODM katika Baraza Jipya la Mawaziri lililotangazwa na Rais William Ruto.
“Tafadhali zingatia kwamba kusalia kwetu katika muungano wa Azimio hakuwezekani kutokana na hali ya kisiasa ya sasa,” alisema kaimu Katibu Mkuu wa chama cha Narc Kenya Asha Bashir katika taarifa.
“Kama chama cha Narc Kenya kupitia barua hii, tunatoa ilani ya kuondoka kwenye muungano kama ilivyoelezwa kwenye kifungu cha kuondoka katika makubaliano ya muungano huo. Ilani hii inaanza kutumika kuanzia tarehe ya kuandikwa,” ilisema taarifa hiyo iliyoandikwa leo Alhamisi, Julai 25, 2024.
Vyama tanzu vya Azimio vikiongozwa na chama cha Wiper chake Kalonzo Musyoka vimekosoa vikali hatua ya kuteuliwa kwa wanachama wa ODM kwa Baraza la Mawaziri.