Home Kimataifa Nangolo Mbumba aapishwa kuwa Rais wa Namibia

Nangolo Mbumba aapishwa kuwa Rais wa Namibia

0

Dkt. Nangolo Mbumba ameapishwa kuwa Rais wa Namibia. 

Hii ni kufuatia kifo cha Rais Hage Geingob mapema jana Jumapili akiwa na umri wa miaka 82.

Shughuli ya kumuapisha Mbumba ambaye amekuwa akihudumu kama Naibu wa Rais iliandaliwa katika ikulu ya Rais jijini Windhoek.

Ilijiri yapata saa 15 tu baada ya kifo cha Hage Geingob ambaye anafahamika sana kwa kushiriki juhudi za ukombozi wa taifa la Namibia.

Katika hotuba yake baada ya kuapishwa, Mbumba alisema kwamba hatawania urais katika uchaguzi mkuu ujao wa mwezi Novemba mwaka huu wa 2024.

Alisema amekubali kuchukua hatamu za uongozi akijua sio jukumu rahisi.

Alitumia fursa hiyo pia kummiminia sifa mtangulizi wake huku akihimiza wananchi kusalia watulivu mipango ya mazishi inapoendelea.

Hage Geingob alifariki alfajiri ya Jumapili, Februari 4, 2024 katika hospitali ya Lady Pohamba alikokuwa akipokea matibabu.

Anasemekana kupatikana akiugua saratani mwaka jana na kwamba alipata matibabu ya kuua seli za saratani kwa muda wa siku mbili nchini Marekani kabla ya kurejea nyumbani Januari 31, 2024.

Website | + posts