Home Habari Kuu Naibu Rais azindua mpango wa mafunzo kwa wanabodaboda

Naibu Rais azindua mpango wa mafunzo kwa wanabodaboda

0

Naibu Rais Rigathi Gachagua leo asubuhi alizindua mpango wa mafunzo kwa waendeshaji pikipiki za kubeba abiria almaarufu bodaboda katika ukumbi wa chuo kikuu cha KEMU jijini Nairobi.

Akizungumza kwenye hafla hiyo, Naibu Rais alisema wako tayari kushirikiana na wanabodaboda kuimarisha usalama kwa kuondoa wahalifu kati yao wanaojisingizia kuwa wafanyabiashara.

Gachagua alisifia sekta ya bodaboda akisema imerahisisha usafiri wa watu na usafirishaji bidhaa. Alisema wanabodaboda ni mashujaa wa uchumi wa nchi hii na sekta yao ni nguzo muhimu kwa uchumi wa taifa.

Mpango huo kwa jina “Boda Yangu, Ofisi Yangu” umefadhiliwa na hazina ya NGAAF kaunti ya Nyandarua kupitia kwa mwakilishi wa wanawake wa kaunti ya Nyandarua, Faith Gitau.

Ni sehemu ya hatua anazotekeleza Gitau katika sekta ya bodaboda. Afisi ya NGAAF kaunti ya Nyandarua inatekeleza mpango huo wa mafunzo kwa ushirikiano na Chuo Kikuu cha Kenya Methodist (KEMU), taasisi ya mafunzo ya kiufundi ya Vera na washikadau wengine.

Wanabodaboda watapata ujuzi kuhusu usalama barabarani, umuhimu wa kujisajili kwenye hazina ya matibabu, NHIF na uwekezaji.

Wawakilishi 265 kutoka wadi zote 25 za kaunti ya Nyandarua watapokea mafunzo hayo na baadaye watakwenda kutoa mafunzo hayo kwa wengine 200 katika kila wadi.

Awamu ya kwanza ya mpango huo inalenga kufikia waendeshaji pikipiki 5,000.

Website | + posts

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here