Home Habari Kuu Naibu Rais afariji familia zilizowapoteza wapendwa wao Maai Mahiu

Naibu Rais afariji familia zilizowapoteza wapendwa wao Maai Mahiu

Zaidi ya watu 45 walipoteza maisha na mali ya mamilioni ya pesa kuharibiwa katika mkasa huo wa siku ya Jumatatu asubuhi.

0

Naibu Rais Rigathi Gachagua, amewataka wakenya kutii maagizo ya kuhamishwa na kuhamia katika maeneo ya juu hasa wakati huu ambapo mvua kubwa inaendelea kunyesha katika maeneo mengi nchini.

Akizungumza alipozifariji familia za watu waliopoteza wapendwa wao Jumatatu alfajiri baada ya bwawa la Old Kijabe kuvunja kingo zake na kumwaga maji katika mji wa Maai Mahiu, naibu Rais aliwasihi wakenya wanaoishi katika maeneo yanayoweza kukabiliwa na maafa kukubaliana kuondoka katika maeneo hayo.

“Wale wanaoishi katika maeneo yanayoweza kumbwa na hatari, wahamie katika maeneo salama. Usisubiri hatari katika nyumba zenu. Tafadhali ondokeni. Usisubiri kifo. Fuateni maagizo kutoka kwa maafisa wa serikali ya taifa, msalaba mwekundu na viongozi wengine,” alisema Gachagua.

Naibu huyo wa Rais alisema manusura wa mkasa huo wa Mai Mahiu, watapewa makazi ya muda mfupi katika shule ya msingi ya Ngeya, iliyo karibu na mji wa Naivasha.

“Tutahakikisha maisha zaidi haipotei. Tutawapatia chakula na bidhaa zingine za msingi. Tutashirikiana na serikali ya kaunti ya Nakuru kuwasaidia manusura kuanza upya maisha,” aliongeza naibu huyo wa Rais.

Zaidi ya watu 45 walipoteza maisha na mali ya mamilioni ya pesa kuharibiwa katika mkasa huo wa siku ya Jumatatu asubuhi.