Home Habari Kuu Naibu Kamanda wa Trafiki Narok afariki katika ajali ya barabarani

Naibu Kamanda wa Trafiki Narok afariki katika ajali ya barabarani

0

Naibu Kamanda wa Trafiki katika kaunti ya Narok Calvin Ochieng ameaga dunia katika ajali ya barabarani kwenye barabara ya Narok kuelekea Bomet.

Ajali hiyo ilitokea katika eneo la Ratili lililoko kaunti ndogo ya Narok Kusini leo Jumatatu asubuhi.

Ochieng alikuwa akiendesha gari lake lenye nambari za usajili KBU 730E akitoka Bomet wakati alipogongana ana kwa ana na lori la kampuni ya Crown Parcel alipokuwa akijaribu kupita lori lingine.

Naibu huyo alipata majeraha mabaya ya miguu na kifua na kufariki papo hapo.

Kamanda wa polisi katika kaunti ya Narok Riko Ngare alithibitisha ajali hiyo akisema kuwa afisa huyo alikuwa akirejea kazini kutoka mashinani wakati alipokumbana na mauti.

Alimtaja afisa huyo kuwa aliyejitolea na kuendesha kazi zake kwa utaratibu unaohitajika.

“Alikuwa akifanya kazi sana barabarani kuhakikisha magari yanapita katika barabara mbalimbali katika mji wa Narok. Ningependa kufikisha salamu zangu za rambirambi kwa familia, marafiki na jeshi zima la polisi,” alisema.

Ngare alitoa wito kwa madereva wa magari kuwa waangalifu wanapoendesha magari kwenye barabara kuu ili kuepusha ajali ambazo zimekuwa zikiongezeka nchini siku za hivi karibuni.

Mwili wa marehemu ulipelekwa katika chumba cha kuhifadhi maiti cha hospitali ya Longisa kwa ajili ya kuhifadhiwa ukisubiri upasuaji kubaini kilichosababisha kifo chake.

Magari yaliyohusika katika ajali hiyo yalikokotwa hadi kituo cha polisi cha Ololulunga kwa uchunguzi zaidi.

Alphas Arap Lagat
+ posts