Naibu Gavana wa kaunti ya Uasin Gishu John Barorot amejiuzulu. Alitangaza kujiuzulu kwake katika mkutano na maafisa wa kaunti hiyo akiwemo Gavana Jonathan Bii, katika hoteli moja jijini Eldoret.
Hatua hii inajiri siku chache tu baada ya Barorot kukanusha uvumi kuhusu kujiuzulu kwake.
Barorot alikosa kuhudhuria hafla ya Rais William Ruto ya kufanya Eldoret kuwa jiji hali iliyosababisha uvumi kusambaa kwamba tayari amejiuzulu.
Wakati huo Barorot alitaja habari hizo kuwa uvumi ila hakuelezea kilichomfanya akose kuhudhuria hafla hiyo muhimu kwa kaunti ya Uasin Gishu.
Kumekuwa na uvumi pia kuhusu kuharibika kwa uhusiano wa kikazi kati ya Gavana Bii na Barorot.
Wakati wa maombi katika makao makuu ya kaunti ya Uasin Gishu yapata wiki tatu zilizopita, Bii alitangaza kwamba Barorot alikuwa likizoni.
Mhandisi Barorot alikosa kwenye maandalizi ya hafla ya kupandishwa hadhi kwa Eldoret kuwa jiji isipokuwa siku moja tu alionekana akisifia vyombo vya habari.
Walipoanza kazi katika uongozi wa kaunti ya Uasin Gishu miaka karibia miwili iliyopita, Bii na Barorot walikuwa wakifanya kazi kwa karibu ambapo walihudhuria hafla mbali mbali pamoja.
Tangazo rasmi la kujiuzulu kwa Barorot linatarajiwa wakati wowote kutoka sasa.