Home Kimataifa Naibu Gavana wa Siaya William Oduol akana tuhuma dhidi yake

Naibu Gavana wa Siaya William Oduol akana tuhuma dhidi yake

0

Naibu Gavana wa kaunti ya Siaya William Oduol amekana tuhuma zote zilizowasilishwa dhidi yake ikiwa ni pamoja na utumiaji mbaya wa wadhifa wake na ukiukaji wa katiba.

Hii ni baada ya Wawakilishi Wadi wote 42 wa bunge la kaunti hiyo kumtimua kufuatia mapendekezo ya jopo la wanachamana 14 lililobuniwa kumchunguza.

Wawakilishi Wadi wanamtuhumu kwa miongoni mwa mambo mengine kukiuka katiba na kupotosha umma kwa kutoa taarifa za uongo.

Ikiwa bunge la Seneti litaidhinisha kutimuliwa kwake, Oduol atakuwa Naibu Gavana wa kwanza kufurushwa ofisini tangu kuasisiwa kwa ugatuzi.

Leo Jumatano, Oduol alifika mbele ya Kamati Maalum ya Seneti inayoongozwa na Seneta William Kisang huku Seneta Betty Batuli Montet akiwa Naibu wake.

Kamati hiyo leo Jumatano ilianza kuandaa vikao vya kusikiliza tuhuma zilizosababisha kutimuliwa kwa Naibu Gavana huyo.

Kulingana na ratiba ya kamati hiyo, kikao cha leo Jumatano kilijumuisha kukongamana kwa pande husika, kujitambulisha kwa wanachama wa Kamati Maalum, kutambulishwa kwa Wawakilishi Wadi wa bunge la Siaya na mawakili wao na wale wa Oduol.

Gavana Orengo na Naibu wake wamekuwa wakivurugana kwa kipindi cha miezi mitatu iliyopita huku Oduol akimnyoshea kidole cha lawama kwa kukimya wakati kukiwa na ubadhirifu wa fedha za umma.

Website | + posts