Home Habari Kuu Naibu Gavana wa Kisii ang’atuliwa mamlakani

Naibu Gavana wa Kisii ang’atuliwa mamlakani

0

Wabunge wa bunge la kaunti ya Kisii wamepiga kura ya kumwondoa afisini naibu Gavana wa kaunti hiyo Daktari Robert Monda.

Wawakilishi wadi 53 waliunga mkono hoja ya kumbandua afisini Monda kwenye mjadala wa Alhamisi Februari 29, 2024 kwa madai ya matumizi mabaya ya mamlaka.

Monda anadaiwa kuhusika kwenye visa vya ulaji rushwa huku akikana mashtaka yote dhidi yake mbele ya bunge hilo mapema leo.

Alisema hakupokea rushwa ili kushawishi kuajiriwa kwa jamaa kwa jina Denis Misati.

Mjadala wa kumbandua mamlakani Monda uliwasilishwa bungeni na mwakilishi wa wadi ya Ichuni Wycliffe Siocha.

Spika wa bunge hilo la kaunti ya Kisii sasa anahitajika kumfahamisha mwenzake wa bunge la Seneti kuhusu hatua hiyo.

Bunge hilo la Seneti litadurusu mchakato mzima kabla ya kikao cha kumsikiliza naibu huyo wa gavana na wakosoaji wake ambao ni bunge la kaunti ya Kisii na baadaye kutoa uamuzi wake.

Hili linaweza kufanyika katika kikao cha bunge zima au katika kikao cha kamati ya muda itakayoteuliwa.

Iwapo bunge la seneti litadumisha uamuzi wa bunge la kaunti basi Monda atapoteza wadhifa huo.

Gavana atakuwa na fursa ya kuteua naibu mwingine ambaye lazima aidhinishwe na bunge la kaunti.

Website | + posts